DKT HUSSEIN OMAR AAHIDI USHIRIKIANO, ACHUKUA MIKOBA YA DKT MAHERA.


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussen Mohamed Omar, ameahidi kushirikiana kwa karibu na watumishi wa wizara hiyo katika kutekeleza majukumu ya sekta ya elimu nchini.



Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi katika makao makuu ya wizara hiyo Mtumba, jijini Dodoma Juni 27, 2025, Dkt. Omar amesema,


“Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini tena. Nitajifunza kutoka kwenu kwani najua wizara hii ina walimu wengi, na natoa ahadi ya ushirikiano wa dhati katika majukumu yetu ya kila siku.”


Dkt. Omar amehamishiwa kutoka Wizara ya Kilimo kuchukua nafasi ya Dkt. Wilson Mahera, ambaye amejiuzulu ili kugombea ubunge katika Jimbo la Butihama, mkoani Mara.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhe. Prof. Carolyne Nombo, amemkaribisha rasmi Dkt. Omar na kueleza kuwa wako tayari kujifunza kutoka kwake kutokana na uzoefu wake katika wizara mbalimbali.



Wizara yetu inafanya kazi kwa karibu na TAMISEMI na taasisi nyingine za elimu, hasa katika kutekeleza sera mpya ya elimu na mitaala iliyo boreshwa. Tunaamini utakuwa msaada mkubwa, amesema Prof. Nombo.


Katika hotuba yake ya kuagana, Dkt. Mahera amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani aliyoionesha kwake kwa kipindi chote cha utumishi wake serikalini.


Dkt. Hussen Omar ni miongoni mwa viongozi walioteuliwa na kufanyiwa mabadiliko ya nafasi na Rais Samia tarehe 23 Juni, 2025. Hafla ya kuwaapisha viongozi hao inatarajiwa kufanyika hivi karibuni.










🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post