Na Saida Issa,Dodoma.
NAIBU Waziri wa fedha Hamad Chande amesema kwa Kifungu cha 10A cha Sheria ya PPP Sura 103 kilianzisha Mfuko wa Uwezeshaji Ubia (PPP Facilitation Fund – PPPFF) kwa lengo la kuziwezesha Mamlaka za Serikali kuandaa na kutekeleza miradi ya PPP.
Naibu huyo ameyaeleza hayo bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Mbeya Vijijini Oran Njeza alipouliza Je, Serikali imewezesha miradi mingapi kwa utaratibu wa ubia wa Serikali na Sekta Binafsi.
Aidha, Kifungu cha 5(1) cha Sheria hiyo imekipa Kituo cha Ubia (PPP Centre) jukumu la kutoa usaidizi wa kiufundi kwa Mamlaka za Serikali na Sekta Binafsi wakati wa uibuaji, maandalizi na utekelezaji wa miradi ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
“Hadi Aprili 2025 jumla ya miradi 80 imewezeshwa na Serikali na ipo katika hatua mbalimbali kama ifuatavyo,
(i) Miradi mitatu (3) ipo katika hatua ya utekelezaji;
(ii) Miradi minne (4) ipo katika hatua ya majadiliano;
(iii) Miradi miwili (2) ipo katika hatua ya ununuzi;
(iv) Miradi 26 ipo katika hatua ya upembuzi yakinifu;
(v) Miradi 13 ipo katika hatua ya upembuzi yakinifu wa awali
(vi) Miradi 32 ipo katika hatua ya andiko dhana,”alisema.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.