Na Carlos Claudio, Dodoma.
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeiomba Serikali kuanzisha sera mahsusi ya kuwatambua na kuwalinda watetezi wa haki za binadamu nchini, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao katika mazingira salama na wezeshi.
Aidha, mtandao huo umeitaka Serikali kufanya mabadiliko katika Sheria ya Mtoto na Sheria ya Msaada wa Kisheria, kwa kuwa sheria hizo ni muhimu katika kulinda haki za makundi maalum ndani ya jamii.
Akifungua mkutano huo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, amesema atawasilisha maombi hayo kwa ajili ya hatua zaidi. Hata hivyo, amesisitiza kuwa mabadiliko yote ya sheria ni vyema yakafanyika kupitia Tume ya Marekebisho ya Sheria Tanzania, ambayo ina mamlaka ya kufanya utafiti na kutoa mapendekezo ya sheria bora kwa ajili ya wananchi.
“Sehemu ya kuwalinda watetezi wa haki za binadamu, mmeandaa sera mfano na nitamfikishia waziri wangu ili liweze kufanyiwa kazi, mabadiliko ya sheria ya mtoto na sheria ya msaada wa kisheria nadhani tulichokuwa tukisisitiza kama wizara na nyakati tofauti tumeshauri mambo mengi tunayojaribu kuwasilisha kupitia Tume ya Marekebisho ya Sheria”,
“Tunapokwenda kimataifa hili sisi ndio linatugusa sana, ukienda nje ya nchi unakuta taarifa imetoka Tanzania imeshachepuka bila waziri mwenye zamana wa eneo hilo haijui, hivi kuna ugomvi gani?” amesema Sagini”.
Nae Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, ametoa maombi katika mkutano huo uliozikutanisha asasi za kiraia na viongozi wa taasisi zinazohusika na usimamizi wa sheria nchini, ambapo amesisitiza umuhimu wa maboresho ya sheria hizo ili kuendana na mahitaji ya sasa ya jamii.
Kwa upande wake Rais wa TLS amesema kuwa wapo teyari kushirikiana na serikali hususani kwenye mambo ya kisheria, kutetea wananchi na kuishauri serikali mambo yanayohusu sheria kwaajili ya kutetea haki za binadamu.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.