Mkazi wa Kijiji cha Kinamweli, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Iddy Renatus Makungu (30), amehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumsababishia ujauzito mwanafunzi wa darasa la nne mwenye umri wa miaka 14.
Hukumu hiyo imesomwa leo Aprili 8, 2025, na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kwimba, Ndeko Dastan Ndeko, ambaye amesema mshtakiwa alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Aprili na Mei 2024, katika Kijiji cha Kinamweli.
Kwa mujibu wa Hakimu Ndeko, mshtakiwa alishtakiwa chini ya Kesi ya Jinai Na. 31962 ya mwaka 2024, kinyume na vifungu vya 130(1) (2) (e) na 131(1) vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya Mwaka 2022.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Juma Kiparo, aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 11, 2024, na kusomewa mashtaka ya ubakaji na kumpa ujauzito mwanafunzi huyo wa Shule ya Msingi Kinamwell, ambapo alikana mashtaka yote mawili.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano, wakiwemo mhanga wa tukio hilo, na Mahakama kujiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa umetosha kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa pasipo kuacha shaka yoyote.
Katika utetezi wake, Makungu alidai kuwa amesingiziwa baada ya kudai malipo ya kazi ya kuchunga ng'ombe aliyokuwa akifanya kwa mjomba wa mhanga.
"Mheshimiwa Hakimu, nimesingiziwa kesi hii baada ya kudai fedha zangu za mshahara nilizokuwa nalipwa kwa kazi ya kuchunga ng'ombe," alijitetea Makungu.
Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali utetezi huo kwa kuwa haukuwa na mashiko, na kumhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka 30 kwa kila kosa, ambapo adhabu hizo zitaenda kwa pamoja. Hivyo, atatumikia kifungo cha miaka 60 jela.