Mahakama ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, imemhukumu Malimo Mathias Nguno (41), maarufu kwa jina la Gohe, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 13 ambaye pia ni mlemavu wa kusikia na kuongea (kiziwi).
Hukumu hiyo imesomwa leo, Aprili 8, 2025, na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ndeko Dastan Ndeko.
Kwa mujibu wa Hakimu Ndeko, mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 130(1) (2) (e) na 131(1) vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022. Kesi hiyo ilikuwa ya jinai namba 2904/2025.
"Baada ya kupitia vifungu vya sheria na kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri, ambao haukuacha shaka yoyote, mahakama hii imekukuta na hatia ya kumbaka mtoto wa kike
mwenye umri wa miaka 13 (jina limehifadhiwa)," amesema Hakimu Ndeko.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, tukio hilo lilitokea Januari 4, 2025, katika Kijiji cha Nyambuyi, ndani ya Wilaya ya Kwimba, ambapo mshtakiwa alimbaka mtoto mwenye ulemavu wa kusikia na kuongea.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Juma Kipalo, amesema kuwa mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Februari 4, 2025, na
kusomewa shtaka la kubaka ambalo alikana mbele ya Mahakama.
Katika kusikiliza kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano, wakiwemo mtaalamu wa lugha za alama na mwalimu wa lugha hiyo aliyesaidia kufanikisha ushahidi wa mhanga mahakamani.
Baada ya kusomewa hukumu, mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali, ambapo aliomba Mahakama impunguzie adhabu akidai umri wake mkubwa na hofu ya kufa gerezani.
Hata hivyo, Hakimu Ndeko alikataa ombi hilo na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela, akisema adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.