MHE. ESTHER MATIKO ASHIRIKI MKUTANO WA 150 WA IPU NCHINI UZBEKISTAN



Pichani ni Mhe. Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, akiwa katika Mkutano wa 150 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaoendelea mjini Tashkent, Uzbekistan.


Mhe. Esther Nicholas Matiko, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Demokrasia na Haki za Binadamu ya IPU, ni miongoni mwa wawakilishi wa Bunge la Tanzania wanaoshiriki katika mkutano huo muhimu unaowakutanisha wabunge kutoka kila kona ya dunia kujadili masuala ya msingi yanayogusa ustawi wa jamii za kimataifa.


Leo, tarehe 8 Aprili 2025, Mhe. Matiko ameshiriki kikao cha Kamati ya Demokrasia na Haki za Binadamu ambapo ajenda kuu imekuwa matumizi ya Akili Bandia (AI) katika muktadha wa demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.


Kikao hicho kimejikita katika kutathmini utekelezaji wa azimio lililopitishwa na IPU mnamo Oktoba 2024 kuhusu changamoto na fursa zinazotokana na maendeleo ya akili bandia.


Katika majadiliano hayo, wajumbe wa Kamati wameonesha wasiwasi juu ya kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya ujasusi bandia (AI surveillance) na athari zake kwa uhuru wa watu, usalama wa taifa, na faragha. Pia wameangazia wajibu wa mabunge katika kutunga sheria madhubuti zitakazolinda haki za binadamu huku zikiwezesha matumizi bora ya teknolojia.


Wabunge kutoka mabunge mbalimbali duniani, akiwemo Mhe. Matiko, wamebadilishana uzoefu na hatua ambazo mabunge yao yamechukua katika kudhibiti au kuhamasisha matumizi ya AI. Vilevile, walijadili changamoto walizokutana nazo, ikiwemo ukosefu wa maarifa ya kutosha kwa baadhi ya wabunge juu ya teknolojia hiyo, na umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuweka kanuni zinazoratibu matumizi ya AI.


Katika kikao hicho, Kamati pia imejadiliana na wataalamu mbalimbali waliotoa tathmini ya kina kuhusu hali ya sasa ya ushirikiano wa kimataifa kuhusu kijasusi bandia, huku wakiangazia namna nchi mbalimbali zinavyoshughulikia suala hilo kwa mujibu wa misingi ya kidemokrasia.


Jambo jingine lililopewa uzito ni namna akili bandiainavyotumika ndani ya mabunge. Wajumbe walijadili matumizi ya AI katika kusaidia kazi za kibunge kama vile uchambuzi wa miswada, kusaidia tafiti kwa ajili ya mijadala, na hata katika kutoa huduma kwa wananchi kupitia mifumo ya dijitali.


Ushiriki wa Mhe. Esther Matiko katika mkutano huu ni uthibitisho wa namna Tanzania inavyotoa mchango wake katika majukwaa ya kimataifa, hasa yale yanayogusa masuala ya msingi kama demokrasia na haki za binadamu. Kupitia mchango wake, Bunge la Tanzania linaendelea kujifunza, kushiriki na kutoa dira kuhusu mustakabali wa matumizi salama na yenye tija ya teknolojia mpya duniani.


Mkutano wa 150 wa IPU unaendelea Tashkent hadi mwishoni mwa juma hili, ambapo wajumbe watakuwa wakijadili pia mada nyingine zinazohusu amani, usawa wa kijinsia, mazingira, na ushirikishwaji wa vijana katika siasa.

Previous Post Next Post