Msemaji wa Serikali ya Iran amesema Mkutano wa
Tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Afrika utafanyika wiki ijayo sambamba na Maonesho ya Saba ya Uwezo wa Biashara ya Nje ya Iran.
Akizungumza na waandishi habari, Bi Fatima Mohajerani amelitaja bara la Afrika kama mojawapo ya masoko makubwa na yenye matumaini makubwa duniani, ambalo linaweza kuwa na mchango muhimu katika kukuza mauzo ya bidhaa zisizo za mafuta kutoka Iran.
Pia amesema maonesho ya "Iran Expo 2025" ni fursa ya kimkakati ya kutambulisha uwezo wa sekta binafsi ya nchi katika kiwango cha kimataifa.
Akiangazia nafasi maalum ya bara la Afrika katika mustakabali wa uchumi wa dunia, ameongeza kuwa Afrika, ikiwa na rasilimali nyingi asili na nguvu kazi, imegeuka kuwa moja ya maeneo muhimu ya uwekezaji wa kimataifa na soko jipya linalochipukia kwa ajili ya bidhaa za nje za nchi mbalimbali.
Aidha amesema kuwa Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Afrika utafanyika tarehe 27 Aprili. Lengo kuu la mkutano huo ni kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa pande mbili na pande nyingi na nchi za Afrika, pamoja na kuweka mazingira ya kusainiwa kwa mikataba ya pamoja kati ya wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Pia alibainisha kuwa kuandaliwa kwa Maonesho ya Saba ya Uwezo wa Biashara ya Nje ya Iran kwa jina la "Iran Expo 2025", kwa wakati mmoja na mkutano wa Iran na Afrika, kunaonyesha kuwa Iran Expo ni jukwaa lenye ufanisi kwa ajili ya kutambulisha uwezo wa uzalishaji na usafirishaji bidhaa nje ya nchi.
Inatarajiwa kuwa wafanyabiashara na wauzaji bidhaa wa kimataifa wapatao kati ya 2,000 hadi 3,000 kutoka nchi mbalimbali wataingia Iran kwa ajili ya kutembelea na kufanya mazungumzo ya kibiashara.
🚨Soma HABARI Zaidi katika BlogSpot yetu ya WASHINDI MEDIA.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.