Kila mwananchi ana jukumu la kumlinda mtu mwenye ulemavu au yule mwenye Mahitaji maalumu bila kujali tofauti kwani watu wote kwenye jamii ni sawa.
Hayo yamebainishwa leo June 29, 2024 na
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ndg. Godfrey Mzava alipotembelea na kugawa zawadi kwa watu wenye makundi maalumu katika kituo cha kulelea watoto kilichopo kwenye shule ya Msingi Bwigiri katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Kiongozi huyo amezungumza na baadhi ya wananchi waliojitokeza katika eneo hilo na kusema kila mwananchi ana wajibu wa kumlinda mwenzake hivyo haipaswi kuwanyanyapaa wala kuwatenga watu wenye mahitaji Maalum kwani nao wana haki ya kuishi kama wengine.
"Kuna baadhi ya watu bado wana imani potofu juu ya watu wenye Ulemavu. Hata Serikali inatambua umuhimu wao kwani wana haki na wajibu kama watu wengine. Tunatakiwa kuhakikisha tuaendelea kuitunza amani ya watu hao"
"Tuendelee kuwalinda kwani wapo maharamia ndani ya nchi hii ambao wanafanya ukatili na utakapoona viashiria hivyo, toa taarifa mapema kwenye vituo vya Polisi vilivyopo karibu yenu" Amesema Mzava.
Haki ya kupata upendo na Amani katika nchi hii ni ya kila mtu bila kujali kabila wala Dini.