WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameshuhudia utiaji saini mikataba 20 ya miradi ya umwagiliaji yenye thamani ya sh. bilioni 258.11 ambayo itatekelezwa kwa kutumia washauri elekezi na wakandarasi wa ndani na wa nje.
Mbali na miradi hiyo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa kutumia wataalam wa ndani, itatekeleza miradi minne yenye thamani ya sh. bilioni 16.95 kwa utaratibu wa Force Account ambayo itakapomilika, inatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya kilimo.
“Kama tulivyoshuhudia, tayari tumekamilisha kusainiwa kwa mikataba ya utekelezaji wa miradi yote 14 ya ujenzi kwa kutumia wakandarasi yenye thamani ya shilingi bilioni 248.76. Vilevile, kuna miradi sita ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kutumia washauri elekezi yenye thamani ya shilingi bilioni 9.35,” amesema.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili 30, 2024) wakati akizungumza na washiriki wa hafla ya utiaji saini wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wabunge, wakuu wa Taasisi zailizo chini ya Wizara ya Kilimo na watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwenye ukumbi wa Mabele, jijini Dodoma.
“Nimefurahi kuona kuwa asilimia 82 ya wakandarasi waliosaini mikataba ni wazawa. Ninampongeza sana Waziri wa Kilimo kwa kusimamia suala hilo. Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa ili kutoa fursa na kuongeza ajira, ujuzi na kipato kwa wazawa.”
“Bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 677 hadi kufikia shilingi bilioni 361.5 mwaka 2023/2024 ikilinganishwa na bajeti ya shilingi bilioni 46.5 iliyotengwa kwa mwaka 2021/2022. Nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya uendelezaji wa miradi ya umwagiliaji nchini.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema utiaji saini wa miradi hiyo unajumuisha hekta 129,792 ambazo zinahusisha ujenzi na usanifu na kwamba ikikamilika itasaidia kuongeza zaidi ya ekari 300,000 kwenye mtandao wa umwagiliaji.