WATAALAMU WAKAGUA MIUNDOMBINU YA MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI WILAYA YA HANANG MKOANI MANYARA

Wataalamu wa Anwani za Makazi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wametembelea Wilaya ya Hanang kukagua Miundombinu ya Anwani za Makazi iliyoharibiwa na maafa yaliyo sababishwa na mafuriko pamoja na maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang yaliyotokea mnamo tarehe 3, Desemba, 2023. 

Maafa hayo yalisababisha madhara makubwa ikiwemo vifo, majeruhi, upotevu wa mali pamoja na uhalibifu wa Miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na miundombinu ya mfumo wa Anwani za Makazi hususan nguzo za majina ya barabara.

Mtaalamu wa Anwani za makazi Bwana Arnold Mkude amesema kuwa lengo la ukaguzi huo ni kuisaidia Serikali kutambua wananchi walioathirika kwa kutumia Anwani za Makazi pamoja na kubainisha miundombinu iliyoharibiwa.

Kutokana na ukaguzi huo, maeneo yaliyobainika kuathirika ni sehemu ya kata ya Kateshi, Gendabi, Jorodom na Ganana ambayo kwa ujumla Anwani za Makazi zipatazo 596 zimeathirika. Vilevile, katika kitongoji cha Katesh stand zaidi ya nguzo 23 za majina ya Barabara zimeharibiwa.

Bwana Mkude amesema kuwa pamoja na kubainisha wananchi walioathirika, hatua za kurejesha miundombinu iliyoharibiwa zinaendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha shughuli za utambuzi wa wananchi zinarudi katika hali yake ya kawaida.

Vile vile, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Jim Yonazi ameishukuru Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Kwa kutuma Wataalamu wa Anwani za Makazi na kusema kuwa wamerahisisha zoezi la  kutambua wananchi walioathirika Kwa Anwani za Makazi.

Previous Post Next Post