DKT.SAMIA NI MUUMINI NAMBA MOJA WA MARIDHIANO NCHINI:DKT.BITEKO

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.  Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni Muumini namba Moja wa maridhiano nchini na haishii katika kusema tu bali anatekeleza kwa vitendo huku nia ikiwa ni kuhakikisha kunakuwa na umoja na amani nchini.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 10 Disemba, 2023 wakati wa Misa Maalum ya Kutabaruku Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT) Lukajange, Dayosisi ya Karagwe iliyofanyika wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera. Misa hiyo maalum imehudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ( CCM), Bara, Komredi Abdulrahman Kinana , Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa.

"Rais,  Dkt. Samia anasema kila mara kuwa hii nchi ni yetu sote, anatuasa mara nyingi kuwa wewe kama ni CCM mpende Mpinzani, na Mpinzani mpende CCM, tuungane pamoja tusukume nchi yetu mbele, na hakuishia hapo tu, akaunda Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano ambayo  imejumuisha makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa kutoka Vyama mbalimbali na viongozi wa dini ili kuwe na muafaka nchini, tujenge Tanzania bora kwa ajili yetu na vizazi vijavyo." Amesisitiza Dkt. Biteko

Ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia amekuwa muumini wa maridhiano si kwa kuigiza bali kwa dhati ya moyo wake na ameonesha mifano mbalimbali ya maridhiano ikiwemo kuwa Mgeni rasmi katika Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) wilayani Moshi na hicho ni kiashirikia kikubwa cha kuonesha kuwa anataka umoja na amani nchini.

vilevile, Dkt. Biteko ameendeelea kusisitiza kuwa, Serikali inaunga mkono madhehebu ya dini na shughuli za kidini nchini na ndiyo maana imeendelea kutoa uhuru wa kuabudu kwa kila mtanzania.

Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko ametaka viongozi mbalimbali nchini kufanya kazi  na watu wanaowaunga mkono na wasiowaunga mkono kwani wajibu wao ni kuwahudumia wananchi wote.


Previous Post Next Post